Important Announcement
PubHTML5 Scheduled Server Maintenance on (GMT) Sunday, June 26th, 2:00 am - 8:00 am.
PubHTML5 site will be inoperative during the times indicated!

Home Explore Mwongozo Nyanya May 2018

Mwongozo Nyanya May 2018

Published by hancy kanda, 2023-08-03 08:12:06

Description: Mwongozo Nyanya May 2018

Keywords: Muongozo Kilimo cha nyanya Nyanya

Search

Read the Text Version

MWONGOZO KILIMO CHA NYANYA KIBIASHARA 1 KilimoSmat Campaign

YALIYOMO MADA UKURASA 1.0 UTANGULIZI.......................................................................................................................... 4 2.0 Hali ya Hewa ...................................................................................................................... 4 3.0 Hali ya Udongo .................................................................................................................. 4 3.1 Aina ya Udongo ............................................................................................................. 4 3.2 Tindikali na Alkali ya Udongo (pH) – Uchachu wa Udongo .................................... 4 4.0 Kitalu cha Nyanya ............................................................................................................. 5 5.0 Uandaaji wa Shamba ....................................................................................................... 5 5.1 Matuta Ya Makingo - Sunken seed beds ................................................................... 5 5.2 Matuta ya kunyanyulia udongo - Raised seed beds ............................................... 6 5.3 Matuta ya Kawaida – Flat seed beds ......................................................................... 6 Ushauri Wetu ............................................................................................................................. 6 6.0 Mbegu za Nyanya ............................................................................................................. 7 6.1 Kotokana na uchavushaji ............................................................................................. 7 6.2 Kutokana na tabia ya ukuaji ........................................................................................ 7 Ushauri Wetu ............................................................................................................................. 7 6.3 Idadi ya Mbegu Kwa Eka.............................................................................................. 8 7.0 Upandaji Mbegu Kwenye Kitalu..................................................................................... 8 Ushauri Wetu ............................................................................................................................. 8 8.0 Uandaaji wa Shamba ...................................................................................................... 9 8.1 Jinsi ya Kuhamisha miche toka Kitaluni kwenda shambani Kitalaamu...............10 8.2 Unatakiwa Upandeje Miche Yako Kitaalamu .........................................................10 8.3 Ni kitu gani Uzingatie Kabla ya Kupanda Miche Shambani .................................11 8.4 Unatakiwa Kutunzaje Shamba lako la Nyanya .......................................................11 8.4.1 Uwekaji wa matandazo (Mulching) ...................................................................11 8.4.2 Kusimika miti ya Kusaidia mmea (Staking)........................................................12 8.5 Umwagiliaji.....................................................................................................................13 Ushauri wetu............................................................................................................................13 2 KilimoSmat Campaign

8.6 Kupalilia..........................................................................................................................13 8.7 Uwekaji wa mbolea ....................................................................................................13 8.8 Magonjwa na Wadudu...............................................................................................14 8.8.1 Wadudu...................................................................................................................14 8.8.2 Magonjwa ..................................................................................................................15 9. 0 Uvunaji na Utunzaji .........................................................................................................17 Ushauri Wetu ...........................................................................................................................18 9.1 Usafirishaji ..........................................................................................................................18 10.0 Masoko ya nyanya ........................................................................................................18 11.0 Bei za nyanya .................................................................................................................19 Ushauri Wetu ...........................................................................................................................20 12. HITIMISHO...........................................................................................................................21 FOMU YA MTEJA – IJAZWE NA MTEJA .................................................................................22 3 KilimoSmat Campaign

1.0 UTANGULIZI Nyanya ni aina ya mboga inayo zalishwa kwa wingi sana duniani. Kwa Tanzania, nyanya ni zao la kwanza katika mazao ya mboga linalo limwa na kuliwa kwa wingi ukilinganisha na mboga zingine. Nyanya hutumika karibu katika kila mlo. Nyanya ni zao umuhimu kama chakula na pia kama zao linalomwingizia kipato mkulima 2.0 Hali ya Hewa Nyanya hustawi vizuri kwenye maeneo ya joto, yasiyo na ukungu mwingi hasa wakati zao linatoa maua na matunda. Zao hili hupenda kipindi kirefu cha jua na joto ili kuongeza ukuaji wa matunda na kupunguza magonjwa ya aina ya ukungu/kuvu. Zao hili halipendi mvua nyingi ingawa linahitaji maji kwa wingi. Katika kipindi chenye mvua nyingi na jua kidogo nyanya hushindwa kutoa maua na matunda ya kutosha bali huweka majani mengi. Katika kipindi hiki pia, nyanya hushambuliwa sana na magonjwa ya ukungu. 3.0 Hali ya Udongo 3.1 Aina ya Udongo Nyanya hustawi kwenye aina zote za udongo kuanzia udongo wa kichanga, mweupe wa tifutifu hadi udongo wa mfinyanzi, ili mradi uwe na mboji ya kutosha na usiosimamisha/tuamisha maji. 3.2 Tindikali na Alkali ya Udongo (pH) – Uchachu wa Udongo Kitalaamu, uchachu wa udongo mzuri kwa nyanya ni ule wa wastani. Uchachu wa wastani ni kati ya pH 6.0 – 7.0. Ofisi za halmashauri za wilaya wanajua Karibu kila eneo wastani wa uchachu ni kiasi gani. Unaweza Kupata maelezo katika Ofisi hizo ama ukapima mwenyewe kwenye maabara mbalimbali. Ofisi yetu unaweza kukusaidia uweze kupima Udongo iwapo utashindwa Kupata huduma hiyo kwa urahisi. 4 KilimoSmat Campaign

4.0 Kitalu cha Nyanya Yapo mambo Matano (5) muhimu ya Kuzingatia katika uandaaji wa Kitalu cha nyanya: i. Kitalu kiwe karibu na maji ya kutosha na ya kudumu. ii. Kiwe sehemu iliyowazi na yenye udongo ulio na rutuba ya kutosha iii. Eneo la kitalu kama ni kubwa liwe tambarare au na mwiinuko kidogo ili kuepuka maji yasituame kwenye kitalu, mteremko ukiwa mkali sana pia sio vizuri kwani husababisha mmomonyoko wa udongo. iv. Kitalu kiwe sehemu ambayo haikuwa na zao la nyanya au viazi mviringo (au mazao ya jamii ya nyanya k.m. mnavu, biringanya n.k.) v. Kiwe sehemu ambayo ni rahisi kupata huduma zote muhimu kwa urahisi, ikiwa ni pamoja na uhamishaji wa miche kwenda sehemu nyingine mfano shambani. 5.0 Uandaaji wa Shamba Shamba la kusia Nyanya inshauriwa liwekwe matutua. Zipo aina tatu za Matuta: i. Matuta ya makingo - Sunken seed beds ii. Matuta ya kunyanyulia Udongo - Raised seed beds iii. Matuta ya kawaida - Flat seed beds 5.1 Matuta Ya Makingo - Sunken seed beds Matuta haya ni rahisi Kutengeneza, hutumika wakati wa kiangazi ili kuhifadhi maji na unyevu unaopatikana ardhini, ni rahisi kumwagilia kwa kutumia maji ya mfereji au bomba, huhifadhi unyevu nyevu kwenye ardhi kwa muda mrefu na huzuia mmomonyoka wa ardhi. Hata hivyo changamoto yake ni kuwa matuta ya namna hii hayawezi kutumika kwenye maeneo yenye mvua nyingi. 5 KilimoSmat Campaign

5.2 Matuta ya kunyanyulia udongo - Raised seed beds Matuta ya namna hii huruhusu maji, hewa na mizizi kupenya kwenye udongo kwa urahisi zaidi, Mazao ya mizizi hupata nafasi ya kutosha kutanuka haraka zaidi, Matuta haya hayatuamishi maji kama mengine, hivyo hutumika zaidi kwenye maeneo yanayokuwa na mvua mara kwa mara. Changamoyo ya aina hii ya matuta ni kuwa yana sababisha sana mmomonyoko wa udongo kama hayakutengenezwa vizuri. 5.3 Matuta ya Kawaida – Flat seed beds Ni rahisi sana kutengeneza matuta ya aina hii kwani udongo ukisha kwatuliwa na kusambazwa mbegu huoteshwa, ni rahisi kutumia eneo kubwa kuotesha Mbegu changamoto yake ni kuwa hayawezi kutumika kwenye maeneo yenye mvua nyingi. Ushauri Wetu Unapoandaa Matuta Zingatia mambo yafuatayo; Tuta liwe na upana kati ya sentimita tisini hadi mia na ishirini (90-120), na urefu wowote ili mradi unaweza kuta huduma biila kukanyaga miche. Kwatua/lima kina kirefu cha kutosha kiasi cha sentimita kumi na tano hadi ishrini (15-20) ili mizizi iweze kusambaa vizuri ardhini. Choma takataka juu ya kitalu, au funika tuta kwa nailoni, majuma manne had inane (4-8) ili kuua vimelea vya magonjwa na wadudu. Wakati wa kuandaa, kitalu, ongeza mbolea aina ya samadi/vunde au mboji kwenye udongo kisha kwatua ili ichanganyike vizuri na udongo. Changanya kiasi cha debe moja (1) hadi mbili (2) kila baada ya mita moja (1) ya mraba. Tuta lisiwe na mabonge-mabonge au mawe-mawe kwani yanaweza kuzuia usambaaji mzuri wa Mbegu. Tuta lisawazishwe vizuri ili kuhakikisha usambazaji mzuri wa mbegu na kuepuka mbegu kufukiwa chini mno kwani zitapata shida Wakati wa kuota. 6 KilimoSmat Campaign

6.0 Mbegu za Nyanya Kuna makundikadhaa ya Mbegu kutokana na uchavushaji na tabia ya ukuwaji kama inavyofafanuliwa hapo chini. 6.1 Kotokana na uchavushaji Kwa kutumia kigenzo cha uchavushaji Nyanya zinagawanyika katika makundi makubwa mawaili kama ifuatavyo: i. OPV (Open Pollinated Variety) – Aina za kawaida. Mfano Tanya, Mwanga, Onyx n.k ii. Hybrid – Chotara: Hizi ni aina zenye mavuno, mengi, zilizoboreshwa zaidi. kati ya hizo zipo aina fupi,za kati na ndefu. Mfano Victory F1, Anna F1, Kipato F1, Monica F1, Kilele F1 n.k/ 6.2 Kutokana na tabia ya ukuaji i. Kutokana na tabia ya ukuahi nyanya zinagawanyika katika makundi matatu kama ifuatavyo; 1. Aina fupi (determinate) kwa mfano Tanya, Cal J, Mwanga, Onyx, Roma VF n.k. Hizi huweza kuvunwa mara 2 hadi 3. ii. Saizi ya Kati. – Hizi ni zile nyanya ndefu kaisi (sio ndefu sana), kitaalamu zinaitwa semi determinate varieties. Mfano wa nyanya aina hii ni Kipato F1. Aina hizi unaweza kuvuna mivuno 3 hadi 5 iii. Aina ndefu ( intermediate) kwa mfano ANNA F1, Victory F1, Tebgeru 97. Aina hizi hufanya vizuri zaidi zinapopandwa ndani ya greenhouse. Uvunaji wake ni wa muda mrefu, kuanzia mivuno 5 na kuendelea, zipo ambazo zinavunwa hata zaidi ya miezi 6, yaani hiyo miezi 6 ni ya uvunaji tu. Ushauri Wetu Kumbuka, Kibiashara, Mbegu za nyanya nzuri ni zile zinazoweza kuvumilia magonjwa, zinazo zaa kwa wingi, na zenye ganda gumu ili kurahisisha usafirishaji na uhifadhi wake. 7 KilimoSmat Campaign

6.3 Idadi ya Mbegu Kwa Eka Utahitaji Mbegu gram 100-150 kwa OPV variety, na Gram 30-50 kwa hybrid - F1. Gharama za kutosha eka moja kwa OPV variety ni Tsh 100,000 hadi 180,000, na kwa Hybrid - F1, Gharama ni kati ya Tsh 200,000 hadi 400,000 kutegemea na aina yenyewe ya mbegu. 7.0 Upandaji Mbegu Kwenye Kitalu Hakikisha Mbegu zako zinaota (germination test) kabla ya kuzipanda Kitaluni. Hivyo Nunua Mbegu kwenye mawakala waliodhibitishwa. Kila pakti ya Mbegu imeandikwa asilimia yake ya kuota (germination percentage) ni vyema Kusoma au kuuliza. Weka mistari kwenye tuta kulingana na ukubwa wa tuta, lakini umbali kati ya mstari na mstari isiwe zaidi ya sentimita kumi na tano hadi ishirini (Sentmita 15-20). Kina cha shimo kisiwe cha kutisha bali kiwe kati ya sentimita Moja hadi Mbili (Sentimita 1-2). Matuta yapate maji ya kutosha siku moja kabla ya kusia mbegu. Ni vizuri kutumia chombo cha kumwagilia, chenye kunyunyiza maji mfano Wotaringken (Watering Cane).Mbegu zipandikizwe kwenye mistari. Changanya mchanga laini na mbegu kisha sambaza kwenye mistari iliyoandaliwa kwenye tuta. Mbegu zinaweza pia kupandwa kwenye tuta bila mistari, lakini zisambazwe kwa uwiano mzuri kwenye tuta ili kupunguza msongamano. Kumbuka msongamano ni chanzo cha Magonjwa kama fangasi mfano Kinyausi (damping off) au Ukungu (Blight). Weka matandazo kiasi cha tosha ili mradi hakitazuia kuota kwa mbegu. Mara baada ya kuatika/kusia mbegu, wagilia maji kiasi cha kutosha kulingana na unyevu nyevu ulioko ardhini Ushauri Wetu Miche ikisha ota, ondoa matandazo, kisha weka chanja ili kupunguza mionzi ya jua ili isiunguze miche michanga japo kwa kipindi cha baridi si muhimu. Punguzia miche (Thinning) ili ipate nafasi ya kutosha angalau miche ibakie kwenye umbali wa sentimita mbili na nusu hadi nne (Sentimita 2.5 – 4). Kwa Kufanya hivyo utapunguza magonjwa ya ulemavu na mnyauko na kupata miche bora yenye nguvu. Endelea 8 KilimoSmat Campaign

kumwagilia hadi miche ifikie kimo kinachofaa kuhamishia shambani. Siku chache kabla ya kuhamishia miche shambani, yaani siku saba hadi kumi (7-10) punguza kiwango cha umwagiliaji maji (hardening). 8.0 Uandaaji wa Shamba Liandaliwe mwezi mmoja hadi miwili (1-2) kabla ya kupanda miche. Mara baada ya kulima choma nyasi juu ya udongo au ondoa magugu yote yanayoweza kuhifadhi wadudu na magonjwa ya nyanya. Siku moja au mbili kabla ya kuhamishia miche ya nyanya shambani, mwagilia sehemu iliyoandaliwa kwa Kupanda nyanya. Nafasi kati ya mche hadi mche ni wastani wa sentimita hamsini hadi sitini au hamsini hadi sabini na tano (50-60) x (50-75) kutegemeana na aina au hali ya hewa. Kama ni kipindi cha baridi ni vyema nyanya zikapandwa mbalimbali ili kuruhusu mzunguko wa hewa na kuzuia magonjwa mbalimbali. 9 KilimoSmat Campaign

8.1 Jinsi ya Kuhamisha miche toka Kitaluni kwenda shambani Kitalaamu i. Mwagilia miche masaa machache kabla ya kuhamishia miche shambani iliwakati wa kung’oa miche mizizi ishikamane vizuri na udongo. ii. Kabla ya kuhamisha miche, mashimo yawe yamekwisha andaliwa katika nafasi zinazo stahili huko shambani. iii. Miche ihamishwe wakati wa jioni ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na jua. iv. Kwa ujumla karibu mazao yote ya mboga mboga huwa tayari kuhamishiwa shambani yakiwa na majani kamili kati ya 2-6 pamoja na mizizi mingi iliyostawi vizuri. v. Mche lazima uwe na afya nzuri, uwe umenyooka vizuri, hivyo miche yote iliyonyongea au myembamba kupita kiasi isichukuliwe wakati wa kupeleka shambani. vi. Ng’oa miche kwa uangalifu hasa pamoja na udongo wake kwa kutumia vifaa husika ili mizizi isidhurike. vii. Miche ihamishiwe shambani mapema mara baada ya kung’olewa toka kitaluni. viii. Wakati wa kuhamisha miche, uangalifu mkubwa utumike ili kutoharibu miche/mizizi. 8.2 Unatakiwa Upandeje Miche Yako Kitaalamu i. Hamisha miche toka kitaluni pamoja na udongo wake ii. Sambaza mizizi vizuri kwenye shimo bila kukunja. iii. Fukia miche kina kile kile ambacho shina lilikuwa limefukiwa bustanini. iv. Mwagilia maji ya kutosha kulingana na unyevunyevu uliopo kwenye udongo kasha weka matandazo na kivuli ili kupunguza uharibifu unaosababishwa na mionzi ya jua. 10 KilimoSmat Campaign

8.3 Ni kitu gani Uzingatie Kabla ya Kupanda Miche Shambani i. Kagua shamba mara kwa mara ili kujua maendeleo au matatizo yaliyoko shambani mapema. ii. Hakikisha shamba ni safi wakati wote, palilia shamba na hakikisha magugu yote hasa yale ya jamii ya nyanya yamelimiwa chini. iii. Ondoa mimea iliyoshambuliwa na magonjwa au ondoa sehemu zilizoshambuliwa, kisha zifukiwe chini au kuunguza moto. iv. Punguza matawi na vikonyo ili kuongeza mwanga wa kutosha kwenye nyanya pamoja na kuruhusu mzunguko wa kutosha wa upepo na kusababisha mazingira magumu ya wadudu maadui kwenye nyanya, hasa wale wanaopenda kiza na magonjwa yanayopendelea unyevunyevu. 8.4 Unatakiwa Kutunzaje Shamba lako la Nyanya 8.4.1 Uwekaji wa matandazo (Mulching) Matandazo yanasaidia kufunika ardhi ili kutunza unyevunyevu, kuzuia magugu, pia matandazo yanasaidia kuzuia matunda ya nyanya yasigusane na udongo ambapo yanaweza kuoza. Matandazo yanaweza kua ya aina mbalimbali, kama vile majani makavu, nyasi au hata maranda yanayatokana na miti wakati wa upasuaji mbao (sawdust). Matandazo ya aina hii ni mzuri zaidi ya yale ya plastiki ambayo sio rahisi kuoza. Matandazo ya nyasi, maranda au maja ni yakioza yanakua mbolea nzuri na kurutubisha ardhi. Uwekaji wa matandazo una 11 KilimoSmat Campaign

ufanisi kwenye kilimo cha eneo dogo, ila kwa maeneo makubwa, upatikanaji wa matandazo unakawa ni changamoto. 8.4.2 Kusimika miti ya Kusaidia mmea (Staking) Uwekaji wa miti/mambo kwa ajili ya kusaidia mmea wa nyanya, kunasaidia nyanya zisianguke au kutambaa kwenye udongo kitu ambacho kinaweza kusababisha madhara kama magonjwa. Miti inapaswa kuwekwa wiki mbili (2) hadi tatu (3) baada ya upandikizaji wa miche. Uwekaji wa miti unasaidia ukuaji wa nyanya na hivyo kupelekea kuzaa zaidi. Kwa aina ndefu za nyanya uwekaji miti hauepukiki ni lazima uweke miti ya kueleweka ambayo itaruhusu ukuwaji mzuri. Kwa nyanya fupi (determinate) na saizi ya kati (Semi determinate) kwa mfano Kipato F1 Tumia fito ndefu japo mita moja na nusu (Mita 1.5) na nene (cm 4-5) pamoja na kamba ngumu mfano kudu/katani. Miti lazima iwe imara ili kuweza kustahimili mzigo wa nyanya pindi itakapokua imezaa vizuri. Nyanya ndefu (indeterminate) mfano victory F1, Anna F1 ni bora zaidi utumie nguzo nene/milunda urefu Mt 2.5 unene sm 10-12 pamoja na waya na kamba nzuri za kudu (tengeneza umbo kama la njia ya umeme). Kabla ya mimea kuweka maua zoezi hili lifanyike. Kusimika Miti Miti Mfano wa Nyaya Za Umeme KilimoSmat Campaign 12

8.5 Umwagiliaji Mavuno yana weza kupungua kwa kiwango kikubwa endapo nyanya zitakosa maji. Nyanya hazivumilii ukame. Ni muhimu kumwagilia mara kwa mara, hasa kama nyanya unalima kipindi cha kiangazi ambapo hakuna mvua. Kiwango cha maji ya umwagiliaji kinategemea aina ya udongo pamoja na hali ya hewa. Udongo wa mfinyazi umwagiliaji ufanyike mara mbili (2) mpaka mara tatu (3) kwa wiki. Udongo wa tifutifu na Kichanga, umwagiliaji ni Mara moja kwa siku. Umwagiliaji ufanyike asubuhi kwa maana mchana mmea ndio unahitaji maji. Ushauri wetu Ni vyema kuangalia hali ya Udongo kabla hujamwagilia. Kama udongo una unyevunyevu wa kutosha, punguza kiasi cha maji au acha kabisai kumwagilia. 8.6 Kupalilia Palizi inapaswa kufanyika wiki 2 au 3 baada ya upandikizaji, ila pia inategemea na uotaji wa magugu katika eneo husika. Hakikisha shamba lako linakua safi bila magugu, maana magugu huvutia na kuficha wadudu na magonjwa. Magugu pia yana uwezo mkubwa wa kutumia virutubisho vilivyomo ardhini kuliko mazao, ndio maana magugu yanakua haraka kuliko mazao shambani. Hivyo hakikisha unafanya palizi mara 3 au 4 kulingana na kasi ya uotaji magugu. 8.7 Uwekaji wa mbolea Mbolea ya kupandia huwekwa wakati wa kupandikiza, unaweka 5g kwenye shimo moja (gramu 5 ni sawa na kifuniko cha soda kimoja). Mbolea ya kupandia unaweza kutumia DAP, MAP, Minjingu n.k. Mbolea ya kukuzia unaweka wiki 2 au 3 baada ya kupandikiza. Ni vizuri mbolea inapowekwa shamba liwe safi, liwe halina magugu, kama kuna magugu fanya palizi kwanza. Mbolea ya kukuzia unaweza kutumia Urea, NPK n.k 13 KilimoSmat Campaign

8.8 Magonjwa na Wadudu 8.8.1 Wadudu Funza washambuliao matunda (Funza wa vitumba): Huyu funza hushambulia mazao mengine kama vile pamba, mahindi, mtama, maharage n.k. Mdudu huyu hushambulia matunda ya nyanya kwa kutoboa na hivyo kuyafanya yapoteze soko kwasababu hayafai kuuzwa katika soko na pia yanaweza kuoza wakati wa usafirishaji. Ili kuthibiti piga dawa ya kuua wadudu kama vile thiodan, sevin ya unga, karate, selecron, n.k. Muarobaini hutumika pia katika kupunguza uharibifu wa dudu huyu. Inzi Mweupe: Wadudu hawa huruka ruka kwenye shamba la nyanya na kukaa chini ya majani. Mdudu huyu hueneza magonjwa ya virusi kama vile “ukoma wa nyanya”. Usafi wa shamba na mazingira ya yake ni muhimu katika kupunguza kuzaana kwa wadudu hawa. Ili kuthibiti wadudu hawa kwenye bustani ya mboga na pia katika maficho yao, piga dawa kama vile karate, cypermethrin mara kwa mara. Panda mimea mingine (kama vile tumbaku) inayo vutia wadudu hawa kwenye maeneo ya bustani kisha piga dawa katika miche ya tumbaku ili uwaangamiza kwa wingi. Minyoo: Mdudu huyu hukaa kwenye udongo wenye unyevu wa kutosha. Huvamia mizizi ya nyanya na kuharibu mfumo wa usafirishaji maji na chakula kwenye nyanya iliyo athirika. Uking'oa mche wa nyanya utaona vifundo kwenye mizizi. Kuzuia Mbinu za kuthibiti ongezeko la wadudu hawa ni kuharibu hali ya udongo inayo mfanya aishi na kuzaana. Mbinu hizi ni: Kulima shamba kwa kutifua baada ya kuvuna nyanya ili udongo wa chini ukae juani na kukauka. Hii inasaidia kuangamiza wadudu hawa kwa joto na ukosefu wa maji. Choma moto na kuteketeza mabaki ya nyanya baada ya kuvuna. kuzungusha aina ya zao la nyanya au jamii ya nyanya na mazao mengine yasiyo vamiwa na adui huyu. Hii huwafanya minyoo wasipate hifadhi na chakula kutoka kwenye mimea wanayo tumia kuishi na kuzaliana. Hivyo idadi yao kupungua katika 14 KilimoSmat Campaign

udongo. Kabla ya kupanda zao weka samadi nyingi katika udongo kwenye eneo lililo athiriwa na wadudu hawa kwani hawapendi udongo wenye samadi nyingi. Panda manung'a nung'a (Tagetes spp) katika eneo lililoathirika na minyoo hawa, mimea hii hutoa sumu ya aina fulani ambayo huathiri ukuaji na kuzaliana kwa minyoo hawa. 8.8.2 Magonjwa Uchunguzi umeonyesha kuwa nyanya na mazao mengine jamii ya nyanya ndiyo hushambuliwa sana na magonjwa kuliko mazao mengine ya mboga. Yafuatayo ni Magonjwa ya Nyanya na dalili zake: Ukukungu: Huu ni ugonjwa unaopenda hali ya unyevu mwingi hewani. Hivyo hujitokeza zaidi wakati wa masika. Pia sehemu zenye umande mwingi wakati wa usiku, ugonjwa huu hujitokeza hata wakati wa kiangazi. Dalili: za ukungu katika nyanya, huu hushambulia shina, maua na matunda. Kuungua kwa majani kama vile yamechomwa na maji moto. Chini ya jani utaona unga unga mweupe. Matunda pia hushambuliwa na ugonjwa huu na hugeuka kuwa meusi na magumu. Jinsi ya Kuzuia: Inabidi kuchanganya mbinu mbali mbali za kupambana na ugonjwa huu. Kwanza ni usafi wa shamba kwa ujumla yaani hakikisha unaondoa magugu katika bustani. Tandaza nyasi juu ya matuta yaliyo pandwa nyanya. Ondoa majani yaliyo zeeka na yanayo onyesha dalili za ugonjwa huu. katika kupunguza majani, hakikisha sehemu za chini ya mmea ni wazi na kuna mzunguko mzuri wa hewa. Punguza majani katika mmea ili kupunguza umande na ukungu kwenye mmea. Baada ya kupunguza majani na machipukizi hakikisha unatupa mbali majani hayo na siyo kuyaacha kwenye tuta la bustani. Ondoa kabisa mmea ulio na dalili za ugonjwa huu. Kupiga dawa katika kipindi cha mvua mara baada ya mvua kubwa. Fanya hivyo mara moja au mara mbili kwa wiki kutegemea na wingi au mfululizo wa mvua. Unapoona jua limetoka piga dawa ili ugonjwa usijitokeze tena. Baadhi ya madawa yanayofaa kukinga ugonjwa huu ni Dithane M45, Bravo, Benlate , Ridomil, Topsin n.k. Kumbuka kuwa kila mwaka madawa yenye nguvu 15 KilimoSmat Campaign

zaidi hutengenezwa, hivyo uliza watalaam walioko karibu nawe. Ingawa Blue Copper inauzwa kwa bei nafuu, nguvu yake in kidogo sana kuthibiti huu ugonjwa. Ushauri Wetu Muarobaini pia unaweza kutumika kupunguza ugonjwa huu. Changanya unga unaotokana na mbegu za muarobaini kiasi cha nusu kilo ya unga katika lita 20 za maji. Ugonjwa wa ukoma wa nyanya: Huu ni ugonjwa wa virus unao enezwa na inzi mweupe. Inzi hawa hushambulia zaidi nyanya wakati wa kiangazi, hasa kipindi cha joto kali. Dalili: Majani machanga hujikunja na baadaye majani yote. Kupungua kwa utoaji maua na matunda na hata yakitokea matunda huwa ni madogo. Mmea kudumaa na kutozaa kabisa. Kuzuia: Mbinu madhubuti ni kupunguza kuenea kwa ugonjwa huu kwenye shamba kwa kudhibiti kuzaana na kuenea kwa mdudu (inzi mweupe) kama tulivyo ona katika kupambana na mdudu huyo, yaani: Kuondoa mimea michache iliyo shikwa na ugonjwa maana wadudu hawa wanachukua ugonjwa huu kutoka mimea hii. Kutumia mbegu zilizo hakikishwa kuwa zinaweza kuvumilia ugonjwa huu na kutoa mavuno mazuri. Usilime nyanya karibu na eneo lililo na mazao kama bamia, mipapai maana mimea hii huhifadhi inzi mweupe. Kuua inzi weupe wanaofyonza nyanya na kusambaza virusi kwa kutumia madawa. Tumia madawa kama vile Selecron, Decis, Karate n.k. Epuka kuchanganya zao la nyanya na mazao mengine yanayohifadhi hawa nzi kama vile mipapai na bamia. Ng'oa na kuchoma moto mimea yote iliyougua ugonjwa huu. Ugonjwa wa mmea wa nyanya kuoza sehemu ya shina inayogusa udongo na mea kunyauka kama vile umekosa maji; Wadudu wanaosabisha ugonjwa huu upatikana ardhini. Hakuna dawa ya kutibu ugonjwa huu baada ya dalili ujitokeza. Kupiga madawa ya viwandani ardhini kabla ya kupanda nyanya husaidia kupungu adudu wa ugonjwa. Epuka kupanda nyanya au mazao jamii ya nyanya katika eneo moja kwa muda mrefu mfulilizo. Baadhi ya mazao yanayohusiana na nyanya ni 16 KilimoSmat Campaign

bilinganya,pilipili,ngogwe,mnavu,n.k. Ugonjwa wa miche michanga ya nyanya kuoza sehemu ya shina inayogusa dongo na kufa ghafla: Ugonjwa huu hushambulia miche kitaluni na husabishwa na wadudu waishio ardhini. Mara baada ya dalili, ugonjwa huu hauna dawa ila unaweza kukingwa kwa kutumia njia zifuatazo; Choma moto udongo wa kutengezea kitalu kabla ya kupanda mbegu zako. Kutumia mboji husaidia kukinga miche dhidi ya ugonjwa huu. Epuka kumwagilia maji kupita kiasi na kutumia kuvuli kizito. Matunda ya nyanya kuoza kitako: Huu ni ugonjwa unaosababishwa na: Umwagiliaji wa nyanya bustanini usio na mpangilio maalumu. Mfano, kumwagilia mimea maji mengi kisha kuiacha bila maji kwa siku kadhaa. Upungufu wa virutubisho aina ya chokaa: Dalili zake ni matunda ya nyanya kuoza sehemu ya kitako na kuonyesha rangi nyeusi. Kuzuia ugonjwa huu, zingatia kuwa na utaratibu mzuri wa kumwagilia maji ambao haubadiliki ovyo kiratiba na kiasi cha maji yanayowekwa. Rutubisha mimea kwa madini ya chokaa kwa kutumia mbolea aina ya CAN zenye madini haya. 9. 0 Uvunaji na Utunzaji Nyanya ina maisha mafupi baada ya kuvunwa, ni rahisi kuharibika maana sehemu kubwa ya nyanya ni maji. Upotevu wa mavuno baada ya kuvuna inakadiriwa kua asilimia 5 hadi 50. Upotevu wa mazao baada ya kuvunwa husababishwa hasa na utunzaji duni wa mazao hayo, njia duni za usafirishaji, pamoja na kuchelewa kuvuna. Kupunguza upotevu unashauriwa kuvuna kwa wakati nyanya zako. Maana nyanya zilizoiva sana, ni rahisi kuharibika wakati wa uvunaji na hata wakati wa kusafirisha maana ganda lake la nje linakua ni laini. Kama soko lako liko mbali vuna nyanya zikiwa ndio zimeanza kuonyesha dalili ya kuiva maana wakati huo nyanya inakua na ganda gumu hivyo kuweza kuvumilia mikikimikiki ya usafirishaji. 17 KilimoSmat Campaign

Ushauri Wetu Mbinu ya kuvuni nyanya kabla ya kuuiva sana inasaidia si tu kuhimili usafiri bali pia kama hujapata soko la uhakika. Nyanya itaweza kukaa muda mrefu zaidi bila kuharibika ikilinganishwa na ile iliyovunwa ikiwa imeiva sana. Kumbuka pia kuna Mbegu zenye uwezo wa kukaa hata wiki tatu (3) zikitunzwa vizuri bila kuharibika. Zingatia kigezo hiki Wakati wa kununua Mbegu. Wakulima Wakipaki Nyanya Kabla ya Kupeleka Sokoni 9.1 Usafirishaji Wakati wa usafirishaji hakikisha unaweka nyanya kwenye vifungashio imara kama kreti ama boksi. Ukiweka kwenye mifuko ni rahisi nyanya kupondeka kutokana na mtikisiko pindi zisafirishwapo hasa kama barabara zenyewe ni za vijijini. 10.0 Masoko ya nyanya Kuna aina kadhaa za masoko ambapo nyanya zinaweza kuuzwa. i. Kuna masoko yasiyo rasmi au masoko ya kawaida (informal markets) kama Kilombero, Arusha, Kariakoo Dar es salaam, soko kuu Morogoro, Buhongwa, Mwanza, na masoko mengine kama hayo yaliyotapakaa nchi nzima. Changamoto ya masoko haya unapitia msururu wa madalali, kila mmoja anataka naye apate. Masoko haya ndiyo yanatumia asilimia kubwa ya nyanya zinazozalishwa. Inakadiriwa kwamba zaidi ya Asilimia 80 ya nyanya zinazozalishwa zinauzwa kwenye masoko hayo. 18 KilimoSmat Campaign

ii. Masoko ya kitaasisi (institutional markets) kama supa markets, mahotelini, hospitali, mashule n.k, Unaweza Kutafuta tenda na kuuza (supply) nyanya kwenye masoko haya. Mfano kama kuna mahoteli unaweza kuyatembelea na kujua wanahitaji nyanya za aina gani, kiasi gani kwa siku au kwa wiki, wanapata wapi nyanya n.k. Kisha ukazalisha kulingana na mahitaji yao ikiwa mtakubaliana. Wapo wakulima wanaohudumia hayo masoko kwa mikataba au kwa kutokua na mikataba. iii. Masoko ya kiviwanda (Industrial markets) kama vile Darsh Industries maarufu kama REDGOLD ambao wako arusha, wao wanazalisha bidhaa nyingi zinazotokana na nyanya kama Tomato Sauce. Pia kipo kiwanda kinaitwa IVORI Iringa kinachotumia nyanya kama malighafi n.k iv. Yapo pia Masoko ya nje ya nchi, soko hili linahitaji ubora wa hali ya juu, ndio maana wachache ndio wanaofaulu kuuza kwenye masoko hayo. Mfano masoko ya nje bidhaa yako lazima ikidhi vigezo vya kimataifa au vya nchi husika. Bado unafursa ya kujifunza kuhusu masoko ya nje na ukaitumia fursa hiyo. 11.0 Bei za nyanya Bei za nyanya zinategemeana na misimu na aina ya soko. Kwenye masoko haya kawaida Bei ya nyanya mara nyingi inakua kubwa kuanzia mwezi wa kumi (October) hadi mwezi Tatu (March) au hata mwezi wa Nne (April). Kipindi cha kuanzia mwezi wa Kumi Na Mbili (December) uzalishaji unakuwa ni mdogo maana watu wachache wanazalisha. Nikipindi chenye changamoto nyingi, kwanza maji ya umwagiliaji yanakua ni tatizo maana wazalishaji wengi wanategemea mvua. Hivyo wale wachache walioko kwenye vyanzo vya maji ndio wanaozalisha. Ipo mikoa kipindi hicho wanapata mvua nyinhi hivyo wadudu na Magonjwa ni mengi, hii hupelekea mavuno kua madogo na gharama za utunzaji nazo ni kubwa. Kipindi hichi bei ya nyanya shambani ni Tsh. 6,000 hadi Tsh 12,000 kwa ndoo ya lita 20. Bei ya sokoni hua ni Tsh 9,000 hadi Tsh 25,000 kwa ujazo wa ndoo ya lita 20. 19 KilimoSmat Campaign

Msimu wa mwezi wa Nne (April) hadi mwezi wa Tisa (September) bei ya nyanya inakua chini, maana uzalishaji ni mkubwa, maeneo mengi hali ya hewa ni nzuri kwa uzalishaji. Kipindi hichi bei ya nyanya ni Tsh 2,000 hadi Tsh 5,000 kwa ndoo ya lita 20. Taasisi ya Mazao ya Mbogambo na Matunda (TAHA), ilitoa bei ya nyanya kwenye masoko mbalimbali nchini mnamo tarehe 13-12-2016 kama ifuatavyo. i. Iringa – Makambako kreti ya kilo 40 ilikuwa Tsh 25,000TSh ii. Tanga – Soweto kreti/tenga ya kilo 40 ilikuwa Tsh 30,000 na Wilayaya Lushoto Tsh 20,000 kwa tenga/kreti Yenye kilo 40. iii. Arusha Tenga (kilo 40) ilikuwa Tsh 28,,000. iv. Mwanza – Kirumba Tenga (Kilo 40) ilikuwa Tsh 20,000 na Dar es Salaam - Kariakoo ilikuwa Tsh 21,300 kwa Tenga la kilo 40. Ile hali Morogoro ilikuwa Tsh 30,000 kwa tenga (kilo 40) v. Zanzibar – Mwanakwerekwe ilikuwa Tsh 45,000 na Dodoma Tsh 60,000 kwa tenga (kilo 40). Na Maeneo ya Kusini Mwa Tanzania, Mtwara na Lindi ilikuwa Tsh 30,000 kwa Tenga la Kilo 40. Ushauri Wetu Hata hivyo pamoja na hayo yote, ili uweze kupenya kwenye soko na kulifaidi soko lazima uwe mbunifu. Kumbuka mjasiriamali haishii tu kufuata soko, balianalitengeneza soko. Jitahidi Kuwa Kupata taarifa mbalimbali kutoka kwenye mashirika na wadau wa Kilimo, udadisi huo nimuhimu ili uweze kuwazidi wenzako, kuwatangulia kwa ubunifu. Mh, Peter Msingwa Mbuge wa Iringa Mjini Mkulima mzuri wa Nyanya 20 KilimoSmat Campaign

2. HITIMISHO Kama ilivyo kwa mazao mengine, Nyanya bora huvutia wanunuzi na huleta faida zaidi. Ubora wa Nyanya unapatikana kwa kutumia mbegu bora na kutunza shamba vizuri kama ilivyo elezwa hapo juu. Ukihitaji msaada zaidi popote pale ulipo, Wasiliana na wataalamu kutoka ofisi ya halmashauri ya Wilaya iliyo karibu nawe. Sisi tupo tayari pia kushirikiana na wewe ili kufanikisha ndoto yako ya kulima Nyanya na kupata faida, tuko tayari kukutembelea shambani kwako na tunakukaribisha ututembelee Ofisini au Kupiga simu ama kutuandikia barua pepe kwa anuani hapo chini ili uwekeze katika Kilimo cha Nyanya na Kupata faida. Tunakutakia maandalizi Mazuri na mafanikio katika Kilimo cha Nyanya. Ofisi Kuu Mwalimu House, Plot No. 48, Block Y, Uhuru/Kawawa Road. 8th Floor, Wing A. P. O. Box 25247 Ilala, Dar es Salaam Tel: +255 (0) 22 220 3171; Cell:, 769 522 222. Email: [email protected] Website: www.mustleadgroup.com 21 KilimoSmat Campaign

FOMU YA MTEJA – IJAZWE NA MTEJA FOMU YA MTEJA Tunafurahi kwa Shauku yako ya Kupata Maarifa ya Kilimo Cha Biashara. Tunapenda kukusaidia zaidi katika mpango wako wa Kilimo Biashara. Ili kufanikisha hilo tunahitaji mawasiliano yako: Jina kamili………………………………………………….. Mkoa…………………………. Wilaya…………………………… Kijiji/Mtaa……………………………….. Simu………………………………………….. Barua pepe……………………………………………. Kitabu umepata kutoka kwa……………………………. Unatarajia Kuanzisha Kilimo Hiki Mwaka………………………………… Kijiji/Mtaa…………………………. Wilaya…………………………Mkoa……………………………… Unatarajia Kuanza na Eka ngapi………………… Sahihi ya Mnunuzi…………………………… Sahihi Muuzaji……………………………. NAMBA YA HUDUMA YA MTEJA (Customer Service Number) ……………………………………………….. ASANTE NA KILA LA KHERI 22 KilimoSmat Campaign


Like this book? You can publish your book online for free in a few minutes!
Create your own flipbook